Colossians 1

Salamu

1 aPaulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, na Timotheo ndugu yetu:

2 bKwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Al-Masihi, waishio Kolosai:

Neema na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu ziwe nanyi.

Shukrani Na Maombi

3 cSiku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, tunapowaombea ninyi, 4 dkwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Al-Masihi Isa, na upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote: 5 eimani na upendo ule utokao katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni, na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani, ile Injili 6 filiyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote. 7 gMlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, yeye aliye mhudumu mwaminifu wa Al-Masihi kwa ajili yenu, 8 hambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho.

9 iKwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 jNasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11 kmkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12 lmkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 mKwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 nambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

Ukuu Wa Al-Masihi

15 oYeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 pKwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 qYeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 rYeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 sKwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20 tna kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.

21 uHapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. 22 vLakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Al-Masihi kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama, 23ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake.

Taabu Ya Paulo Kwa Ajili Ya Kanisa

24 wSasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Al-Masihi kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa. 25 xMimi nimekuwa mtumishi wa kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu: 26 yHii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. 27 zKwao, Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Al-Masihi ndani yenu, tumaini la utukufu.

28 aaYeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Al-Masihi. 29 abKwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.
Copyright information for SwhKC